\h MATENDO
MATENDO YA MITUME
\c 1
1 Ndugu Theofilo,
\m Katika kitabu cha kwanza niliandika juu ya mambo yote Yesu aliyotenda
na kufundisha tangu mwanzo wa kazi yake
2 mpaka siku ile alipochukuliwa mbinguni. Kabla ya kuchukuliwa
mbinguni aliwapa maagizo kwa njia ya Roho Mtakatifu wale mitume
aliowachagua.
3 Kwa muda wa siku arobaini baada ya kifo chake aliwatokea mara
nyingi kwa namna ambazo zilithibitisha kabisa kwamba alikuwa hai.
Walimwona, naye aliongea nao juu ya ufalme wa Mungu.
4 Wakati walipokutana pamoja aliwaamuru hivi: “Msiondoke
Yerusalemu, bali ngojeeni ile zawadi aliyoahidi Baba, zawadi ambayo
mlikwisha nisikia nikiongea juu yake.
5 Kwani Yohane alibatiza kwa maji, lakini baada ya siku chache,
ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.”
Yesu anapaa mbinguni
6 Basi, mitume walipokutana pamoja na Yesu, walimwuliza, “Je Bwana,
wakati huu ndipo utakaporudisha ule ufalme kwa Israeli?”
7 Lakini Yesu akawaambia, “Nyakati na majira ya mambo hayo viko
chini ya mamlaka ya Baba yangu, wala si shauri lenu kujua yatakuwa lini.
8 Lakini wakati Roho Mtakatifu atakapowashukieni ninyi, mtajazwa
nguvu na mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, katika nchi yote ya
Yudea na Samaria, na hata miisho ya dunia.”
9 Baada ya kusema hayo, wote wakiwa wanamtazama, alichukuliwa
mbinguni; wingu likamficha wasimwone tena.
10 Walipokuwa bado wanatazama juu angani, akiwa anakwenda zake, mara
watu wawili waliokuwa wamevaa nguo nyeupe walisimama karibu nao,
11 wakasema, “Enyi wananchi wa Galilaya! Mbona mnasimama mkitazama
angani? Yesu huyu ambaye amechukuliwa kutoka kwenu kwenda mbinguni
atakuja tena namna hiyohiyo mliivyomwona akienda mbinguni.”
Mathia anachaguliwa ashike nafasi ya Yuda
12 Kisha mitume wakarudi Yerusalemu kutoka mlima wa Mizeituni ulioko
karibu kilomita moja kutoka mjini.
13 Walipofika mjini waliingia katika chumba ghorofani ambamo
walikuwa wanakaa; nao walikuwa Petro, Yohane, Yakobo, Andrea, Filipo na
Thoma, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni Zelote na
Yuda mwana wa Yakobo.
14 Hawa wote walikusanyika pamoja kusali, pamoja na wanawake kadha
wa kadha, na Maria mama yake Yesu, na ndugu zake.
15 Siku chache baadaye, kulikuwa na mkutano wa waumini, karibu watu
mia moja na ishirini. Petro alisimama mbele yao,
16 akasema, “Ndugu zangu, ilikuwa lazima ile sehemu ya Maandiko
Matakatifu itimie, sehemu ambayo Roho Mtakatifu, kwa maneno ya Daudi,
alibashiri habari za Yuda ambaye aliwaongoza wale waliomtia Yesu
nguvuni.
17 Yuda alikuwa mmoja wa kikundi chetu maana alichaguliwa ashiriki
huduma yetu.
(((
18 “Mnajua kwamba yeye alinunua shamba kwa zile fedha alizopata
kutokana na kitendo chake kiovu. Akaanguka chini, akapasuka na matumbo
yake yakamwagika nje.
19 Kila mtu katika Yerusalemu alisikia habari za tukio hilo na
hivyo, kwa lugha yao, wakaliita lile shamba <Hekeli Dama>, maana yake,
<Shamba la Damu.>)
20 Basi, imeandikwa katika kitabu cha Zaburi:
<Nyumba yake ibaki mahame;
mtu yeyote asiishi ndani yake.>
\m Tena imeandikwa:
<Mtu mwingine achukue nafasi yake katika huduma hiyo.>
\m
21-22 Kwa hiyo, ni lazima mtu mwingine ajiunge nasi kama shahidi wa
ufufuo wake Bwana Yesu. Anapaswa kuwa mmoja wa wale waliokuwa katika
kundi letu wakati wote Bwana alipokuwa anasafiri pamoja nasi, tangu
wakati Yohane alipokuwa anabatiza mpaka siku ile Yesu alipochukuliwa
kutoka kwetu kwenda mbinguni.”
23 Basi, wakataja majina ya watu wawili; wa kwanza Yosefu aliyeitwa
Barsaba (au pia Yusto), na wa pili Mathia.
24 Kisha wakasali: “Bwana, wewe unajua mioyo ya watu wote. Hivyo,
utuonyeshe ni yupi kati ya hawa wawili uliyemchagua
25 ili achukue nafasi hii ya huduma ya kitume aliyoacha Yuda akaenda
mahali pake mwenyewe.”
26 Hapo, wakapiga kura; kura ikampata Mathia, naye akaongezwa katika
idadi ya wale mitume wengine kumi na mmoja.
\c 2
Roho Mtakatifu anawashukia waumini
1 Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika
pamoja.
2 Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya
upepo mkali, ikajaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa.
3 Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto,
vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali
kadiri Roho alivyowawezesha.
5 Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu,
waliotoka katika kila nchi duniani.
6 Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote
walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa
lugha yake mwenyewe.
7 Walistaajabu na kushangaa, wakisema, “Je, hawa wote tunaowasikia
wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?
8 Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa
lugha yake mwenyewe?
9 Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa
Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,
10 Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene;
wengine wetu ni wageni kutoka Roma,
11 Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka
Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe
mambo makuu ya Mungu.”
12 Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, “Hii ina maana
gani?”
13 Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, “Watu hawa wamelewa divai
mpya!”
Hotuba ya Petro
14 Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza
kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: “Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa
hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.
15 Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu
asubuhi?
16 Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
17 <Katika siku zile za mwisho, asema Bwana,
nitawamiminia binadamu wote Roho wangu.
Watoto wenu, wanaume kwa wanawake,
watautangaza ujumbe wangu;
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
nitawamiminia Roho wangu, siku zile,
nao watautangaza ujumbe wangu.
19 Nitatenda miujiza juu angani,
na ishara chini duniani;
kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
20 jua litatiwa giza,
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
21 Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.>
22 “Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti
alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa
miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake,
kama mnavyojua.
23 Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba
Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya
wamsulubishe.
24 Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika maumivu ya
kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.
25 Maana Daudi alisema juu yake hivi:
<Nilimwona Bwana mbele yangu daima;
yuko nami upande wangu wa kulia,
na hivyo sitatikisika.
26 Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi;
tena nilipiga vigelegele vya furaha.
Mwili wangu utakaa katika tumaini;
27 kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu,
wala kumruhusu mtakatifu wako aoze.
28 Umenionyesha njia za kuufikia uzima,
kuwako kwako kwanijaza furaha!>
29 “Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo
yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake
liko papa hapa petu mpaka leo.
30 Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia
kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake.
31 Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema
juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: <Hakuachwa kuzimu, mwili wake
haukuoza.>
32 Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa
tukio hilo.
33 Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu, akapokea
kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona
sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho.
34 Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema:
<Bwana alimwambia Bwana wangu:
Keti upande wangu wa kulia,
35 hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia miguu yako.>
36 “Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo
Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana
na Kristo.”
37 Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro
na wale mitume wenzake: “Ndugu zetu, tufanye nini?”
38 Petro akajibu, “Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la
Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi ya
Roho Mtakatifu.
39 Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto
wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye
Bwana Mungu wetu atamwita kwake.”
40 Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu
akisema, “Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu.”
41 Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu
tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.
42 Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja
kidugu, kumega mkate na kusali.
Maisha ya kila siku ya wale waumini
43 Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila
mtu akajawa na hofu.
44 Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana
pamoja.
45 Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri
ya mahitaji ya kila mmoja.
46 Waliendelea kukutana pamoja kila siku Hekaluni. Lakini wakati wa
kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula
hicho kwa furaha na moyo mkunjufu.
47 Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana
aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.
\c 3
Petro na Yohane wanamponya kiwete mmoja
1 Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wanakwenda
Hekaluni, wakati wa sala.
2 Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao “Mlango Mzuri”,
palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo mtu
kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa
wakiingia Hekaluni.
3 Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba wampe
chochote.
4 Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia,
“Tutazame!”
5 Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.
6 Kisha Petro akamwambia, “Sina fedha wala dhahabu lakini kile
nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!”
7 Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na
magoti yake yakapata nguvu.
8 Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao
Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.
9 Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.
10 Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule
“Mlango Mzuri” wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa
yaliyompata.
Hotuba ya Petro
11 Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali
palipoitwa “Ukumbi wa Solomoni,” ambapo yule mtu alikuwa bado
anaandamana na Petro na Yohane.
12 Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, “Wananchi wa
Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho
kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya
mtu huyu aweze kutembea?
13 Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza
Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na
kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.
14 Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu
mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.
15 Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu
alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.
16 Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu
mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya
kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.
17 “Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda
hayo kwa sababu ya kutojua kwenu.
18 Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa
njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.
19 Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu.
20 Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na
kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.
21 Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa
kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake
watakatifu wa tangu zamani.
22 Kwa maana Mose alisema, <Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii
kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe.
23 Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na
watu wa Mungu na kuangamizwa.>
24 Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza
habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi.
25 Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu;
na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama
alivyomwambia Abrahamu: <Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia
zitabarikiwa.>
26 Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua
mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane
kabisa na maovu yake.”