UFUNUO ALIOPEWA

YOHANE
\h UFUNUO
\c 1

1 Hizi ni habari za mambo ambayo yalifunuliwa na Yesu Kristo. Mungu
alimpa Kristo ufunuo huu ili awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo
yanapaswa kutukia karibuni. Kristo alimtuma malaika wake amjulishe
Yohane, mtumishi wake, mambo hayo,
2 naye Yohane, ameyasema yote aliyoyaona. Na hii ndio taarifa yake
kuhusu ujumbe wa Mungu na ukweli uliofunuliwa na Yesu Kristo.
3 Heri yake mtu anayesoma kitabu hiki; heri yao wale wanaosikiliza
maneno ya ujumbe huu wa kinabii na kushika yaliyoandikwa humu, maana
wakati umekaribia ambapo mambo haya yatatukia.

Salamu kwa makanisa saba

4 Mimi Yohane nayaandikia makanisa yaliyoko mkoani Asia. Nawatakieni
neema na amani kutoka kwake yeye aliyeko, aliyekuwako na anayekuja; na
kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi,
5 na kutoka kwa Yesu Kristo, shahidi mwaminifu, wa kwanza kufufuliwa
kutoka wafu, na ambaye ni mtawala wa wafalme wa dunia.
\fr 1:5
\f taz Zab 89:27
Yeye anatupenda, na kwa damu yake ametufungua kutoka vifungo vya
dhambi zetu,
6 akatufanya sisi kuwa ufalme wa makuhani, tumtumikie Mungu, Baba
yake. Kwake Yesu Kristo uwe utukufu na nguvu, milele na milele! Amina.

7 Tazama! Anakuja katika mawingu! Kila mtu atamwona, hata wale
waliomchoma. Makabila yote duniani yataomboleza juu yake. Naam! Amina.

8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu Mwenye Uwezo,
aliyeko, aliyekuwako na anayekuja.

Njozi ya Mwana wa Mtu

9 Mimi ni Yohane, ndugu yenu; na kwa kuungana na Kristo nashiriki
pamoja nanyi katika kustahimili mateso yanayowapata wale walio wa
Utawala wake. Mimi nilikuwa kisiwani Patmo kwa sababu ya kuhubiri ujumbe
wa Mungu na ukweli wa Yesu.
10 Basi, wakati mmoja, siku ya Bwana, nilikumbwa na Roho, nikasikia
nyuma yangu sauti kubwa kama sauti ya tarumbeta.
11 Nayo ilisema, “Andika katika kitabu yote unayoyaona, ukipeleke
kwa makanisa haya saba: Efeso, Smurna, Pergamoni, Thuatira, Sarde,
Filadelfia na Laodikea.”

12 Basi, nikageuka nimwone huyo aliyesema nami, nikaona vinara vya
taa saba vya dhahabu,
13 na katikati yake kulikuwa na kitu kama mtu, naye alikuwa amevaa
kanzu ndefu na ukanda wa dhahabu kifuani.
14 Nywele zake zilikuwa nyeupe kama pamba safi, kama theluji; macho
yake yalimetameta kama moto;
15 miguu yake iling’aa kama shaba iliyosafishwa katika tanuru ya
moto na kusuguliwa, na sauti yake ilikuwa, kama sauti ya poromoko la
maji.
16 Katika mkono wake wa kulia, alikuwa na nyota saba, na kinywani
mwake mlitoka upanga wenye makali kuwili. Uso wake uling’aa kama jua
kali.

17 Basi, nilipomwona tu, nilianguka mbele ya miguu yake kama maiti.
Lakini yeye akaweka mkono wake wa kulia juu yangu, akasema, “Usiogope!
Mimi ni wa kwanza na wa mwisho.
18 Mimi ni yeye aliye hai! Nilikuwa nimekufa, lakini, tazama, sasa
ni mzima milele na milele. Ninazo funguo za kifo na Kuzimu.
19 Basi, sasa andika mambo haya unayoyaona, mambo yanayotukia sasa
na yale yatakayotukia baadaye.
20 Siri ya nyota zile saba ulizoziona katika mkono wangu wa kulia,
na siri ya vile vinara saba vya taa hii: zile nyota saba ni malaika wa
makanisa; na vile vinara saba vya taa ni makanisa saba.

\c 2

Ujumbe kwa Efeso

1 “Kwa malaika wa kanisa la Efeso andika hivi:
“Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye ashikaye nyota saba katika mkono
wake wa kulia, na ambaye hutembea katikati ya vinara saba vya taa vya
dhahabu.
2 Najua mambo yako yote; najua bidii yako na uvumilivu wako. Najua
kwamba huwezi kuwavumilia watu waovu, na kwamba umewapima wale
wanaojisemea kuwa mitume na kumbe sio, ukagundua kwamba ni waongo.
3 Wewe unayo saburi, umestahimili taabu nyingi kwa ajili ya jina
langu, wala hukuvunjika moyo.
4 Lakini ninayo hoja moja juu yako: wewe hunipendi tena sasa kama
pale awali.
5 Basi, pakumbuke pale ulipokuwa kabla ya kuanguka, ukayaache
madhambi yako, na kufanya kama ulivyofanya pale awali. La sivyo, naja
kwako na kukiondoa kinara chako mahali pake.
6 Lakini nakusifu juu ya kitu kimoja: wewe unayachukia wanayoyatenda
Wanikolai kama ninavyoyachukia mimi.

7 “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!
“Wale wanaoshinda nitawapa haki ya kula matunda ya mti wa uzima
ulioko ndani ya bustani ya Mungu.

Ujumbe kwa Smurna

8 “Kwa malaika wa kanisa la Smurna andika hivi:
“Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye wa kwanza na wa mwisho, ambaye
alikufa na akaishi tena.
9 Najua taabu zako; najua pia umaskini wako, ingawaje kwa kweli wewe
ni tajiri; najua kashfa walizokufanyia wale wanaojiita Wayahudi lakini
si Wayahudi wa kweli, bali ni kundi lake Shetani.
10 Usiogope hata kidogo yale ambayo itakulazimu kuteseka. Sikiliza!
Ibilisi anataka kuwajaribu kwa kuwatia baadhi yenu gerezani; nanyi
mtapata dhiki kwa muda wa siku kumi. Muwe waaminifu hata mpaka kufa,
nami nitawapeni taji ya uzima.

11 “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!
“Wale wanaoshinda hawataumizwa na kifo cha pili.

Ujumbe kwa Pergamoni

12 “Kwa malaika wa kanisa la Pergamoni andika hivi:
“Huu ndio ujumbe wake yeye aliye na upanga mkali wenye kuwili.
13 Najua unakoishi: Wewe unaishi kwenye makao makuu ya Shetani!
Lakini bado unashikilia jina langu; hukuikana imani yako kwangu hata
siku zile Antipa shahidi wangu mwaminifu, alipouawa pale mahali
anapoishi Shetani.
14 Lakini ninayo machache dhidi yako: baadhi yenu ni wafuasi wa
Balaamu aliyemfundisha Balaki kuwatega wana wa Israeli wale vyakula
vilivyotambikiwa sanamu za kufanya uzinzi.
15 Vivyo hivyo, wako pia miongoni mwenu watu wanaofuata mafundisho
ya Wanikolai.
16 Basi, achana na madhambi yako. La sivyo, nitakuja kwako upesi na
kupigana na watu hao kwa upanga utokao kinywani mwangu.

17 “Aliye na masikio, basi, na asikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!
“Wale wanaoshinda nitawapa ile mana iliyofichika. Nitawapa pia jiwe
jeupe lililoandikwa jina jipya ambalo hakuna mtu aliyelijua isipokuwa tu
wale wanaolipokea.

Ujumbe kwa Thuatira

18 “Kwa malaika wa kanisa la Thuatira andika hivi:
“Huu ndio ujumbe wa Mwana wa Mungu, ambaye macho yake yametameta
kama moto, na miguu yake inang’aa kama shaba iliyosuguliwa.
19 Najua mambo yako yote. Najua upendo wako, imani yako, utumishi
wako na uvumilivu wako. Wewe unafanya vizuri zaidi sasa kuliko pale
awali.
20 Lakini nina hoja moja juu yako: wewe unamvumilia yule mwanamke
Yezabeli anayejiita nabii wa Mungu. Yeye huwafundisha na kuwapotosha
watumishi wangu wafanye uzinzi na kula vyakula vilivyotambikiwa sanamu.
21 Nimempa muda wa kutubu dhambi zake, lakini hataki kuachana na
uzinzi wake.
22 Sikiliza! Sasa namtupa kitandani ambapo yeye pamoja na wote
waliofanya uzinzi naye watapatwa na mateso makali. Naam, nitafanya
hivyo, kama wasipotubu matendo yao mabaya waliyotenda naye.
23 Tena nitawaua wafuasi wake, ili makanisa yote yatambue kwamba
mimi ndiye ninayechunguza mioyo na fikira za watu.
\fr 2:23
\f taz Zab 7:9; 62:12

24 “Lakini ninyi wengine mlioko huko Thuatira ambao hamfuati
mafundisho yake Yezabeli, na ambao hamkujifunza kile wanachokiita <Siri
ya Shetani>, nawaambieni kwamba sitawapeni mzigo mwingine.
25 Lazima mzingatie yale mliyo nayo sasa mpaka nitakapokuja.

26-28 “Wanaoshinda, na wale watakaozingatia mpaka mwisho kutenda
ninayotaka, nitawapa mamlaka juu ya mataifa. Naam, nitawapa uwezo uleule
nilioupokea kwa Baba: yaani, watayatawala mataifa kwa fimbo ya chuma na
kuyavunjavunja kama chombo cha udongo. Tena nitawapa nyota ya asubuhi.
\fr 2:26-27
\f taz Zab 2:8-9

29 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!

\c 3

Ujumbe kwa Sarde

1 “Kwa malaika wa kanisa la Sarde andika hivi:
“Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye na roho saba za Mungu na
nyota saba. Nayajua mambo yako yote; najua unajulikana kuwa na uhai
kumbe umekufa!
2 Amka! Imarisha chochote chema kilichokubakia kabla nacho
hakijatoweka kabisa. Maana, mpaka sasa, sijayaona matendo yako kuwa ni
makamilifu mbele ya Mungu wangu.
3 Kumbuka, basi, yale uliyofundishwa na jinsi ulivyoyasikia, uyatii
na ubadili nia yako mbaya. Usipokesha nitakujia ghafla kama mwizi, na
wala hutaijua saa nitakapokujia.
4 Lakini wako wachache huko Sarde ambao hawakuyachafua mavazi yao.
Hao wanastahili kutembea pamoja nami wakiwa wamevaa mavazi meupe.

5 “Wale wanaoshinda, watavikwa mavazi meupe kama hao. Nami
sitayafuta majina yao kutoka katika kitabu cha uzima; tena nitawakiri
kwamba ni wangu mbele ya Baba yangu na mbele ya malaika wake.
\fr 3:5
\f taz Zab 69:28

6 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!

Ujumbe kwa Filadelfia

7 “Kwa malaika wa kanisa la Filadelfia andika hivi:
“Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aliye mtakatifu na wa kweli,
ambaye anao ule ufunguo wa Daudi, na ambaye hufungua na hakuna mtu
awezaye kufungua.
8 Nayajua mambo yako yote! Sasa, nimefungua mbele yako mlango ambao
hakuna mtu awezaye kuufunga; najua kwamba ingawa huna nguvu sana, hata
hivyo, umezishika amri zangu, umelitii neno langu wala hukulikana jina
langu.
9 Sikiliza! Nitawapeleka kwako watu wa kundi lake Shetani, watu
ambao hujisema kuwa ni Wayahudi, kumbe ni wadanganyifu. Naam,
nitawapeleka kwako na kuwafanya wapige magoti mbele yako wapate kujua
kwamba kweli nakupenda wewe.
10 Kwa kuwa wewe umezingatia agizo langu la kuwa na uvumilivu, nami
pia nitakutegemeza salama wakati ule wa dhiki inayoujia ulimwengu mzima
kuwajaribu wote wanaoishi duniani.
11 Naja kwako upesi! Linda, basi, ulicho nacho sasa, ili usije
ukanyang’anywa na mtu yeyote taji yako ya ushindi.

12 “Wale wanaoshinda nitawafanya wawe minara katika Hekalu la Mungu
wangu, na hawatatoka humo kamwe. Pia nitaandika juu yao jina la Mungu
wangu na jina la mji wa Mungu wangu, yaani Yerusalemu mpya, mji ambao
utashuka kutoka juu mbinguni kwa Mungu wangu. Tena nitaandika juu yao
jina langu jipya.

13 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!

Ujumbe kwa Laodikea

14 “Kwa malaika wa kanisa la Laodikea andika hivi:
“Huu ndio ujumbe kutoka kwake yeye aitwaye <Amina>. Yeye ni shahidi
mwaminifu na wa kweli, ambaye ni chanzo cha viumbe vyote alivyoumba
Mungu.
15 Nayajua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wala si
moto. Afadhali ungekuwa kimojawapo: baridi au moto.
16 Basi, kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto,
nitakutapika!
17 Wewe unajisema, <Mimi ni tajiri; ninajitosheleza, sina haja ya
kitu chochote.> Kumbe, hujui kwamba wewe ni mnyonge, unahitaji
kuhurumiwa, maskini, kipofu tena uko uchi!
18 Nakushauri ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto upate
kuwa tajiri kweli. Tena afadhali ununue pia vazi jeupe, uvae na kufunika
aibu ya uchi wako. Nunua pia mafuta ukapake machoni pako upate kuona.
19 Mimi ndiye mwenye kumwonya na kumrudi yeyote ninayempenda. Kwa
hiyo kaza moyo, achana na dhambi zako.
20 Sikiliza! Mimi nasimama mlangoni na kubisha hodi. Mtu akisikia
sauti yangu na kufungua mlango, nitaingia nyumbani kwake na kula chakula
pamoja naye, naye atakula pamoja nami.

21 “Wale wanaoshinda nitawaketisha pamoja nami juu ya kiti changu
cha enzi, kama vile mimi mwenyewe nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba
yangu juu ya kiti chake cha enzi.

22 “Aliye na masikio, basi, na ayasikie yale Roho anayoyaambia
makanisa!”

\c 4

Ibada mbinguni

1 Baada ya hayo nilitazama nikaona mlango umefunguliwa mbinguni. Na
ile sauti niliyoisikia pale awali ambayo ilikuwa kama sauti ya
tarumbeta, ikasema, “Njoo hapa juu nami nitakuonyesha mambo
yatakayotukia baadaye.”
2 Mara nikachukuliwa na Roho. Kumbe, huko mbinguni kuna kiti cha
enzi na juu yake ameketi mmoja.
3 Huyo aliyeketi juu yake alikuwa kama almasi na jiwe zuri jekundu.
Upinde wa mvua ulikuwa unang’aa kama zumaridi na ulikizunguka kiti cha
enzi pande zote.
4 Kulikuwa na duara la viti ishirini na vinne kukizunguka kiti cha
enzi, na juu ya viti hivyo wazee ishirini na wanne walikuwa wameketi
wamevaa mavazi meupe na taji za dhahabu vichwani.
5 Umeme, sauti na ngurumo, vilikuwa vinatoka kwenye hicho kiti cha
enzi. Taa saba za moto zilikuwa zinawaka mbele ya hicho kiti cha enzi.
Taa hizo ni roho saba za Mungu.
6 Mbele ya kiti cha enzi kulikuwa na kitu kama bahari ya kioo,
angavu kama jiwe linga’aalo sana.
Katika pande zote za hicho kiti cha enzi na kukizunguka, kilikuwa na
viumbe hai vinne. Viumbe hivyo vilikuwa vimejaa macho mbele na nyuma.
7 Kiumbe cha kwanza kulikuwa kama simba, cha pili kama ng’ombe, cha
tatu kilikuwa na sura kama mtu, na cha nne kilikuwa kama tai anayeruka.
8 Viumbe hivyo vinne vilikuwa na mabawa sita kila kimoja, na
vilikuwa vimejaa macho, ndani na nje. Usiku na mchana, bila kupumzika
huimba:

“Mtakatifu, mtakatifu, mtakatifu
ni Bwana, Mungu Mwenye Uwezo,
aliyekuwako, aliyeko na anayekuja!”

9 Kila mara viumbe vinne vilipoimba nyimbo za kumtukuza, kumheshimu
na kumshukuru huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi, ambaye anaishi milele
na milele,
10 wale wazee ishirini na wanne hujiangusha mbele ya huyo aliyeketi
juu ya kiti cha enzi na kumwabudu huyo ambaye anaishi milele na milele;
na huziweka taji zao mbele ya kiti cha enzi wakisema:

11 “Wewe ni Bwana na Mungu wetu,

unastahili utukufu na heshima na nguvu;
maana wewe uliumba vitu vyote,
na kwa matakwa yako kila kitu kimepewa uhai na uzima.”

\c 5

Kitabu na Mwanakondoo

1 Kisha katika mkono wa kulia wa huyo aliyeketi juu ya kiti cha enzi,
nikaona kitabu; nacho kilikuwa kimeandikwa ndani na nje na kufungwa na
mihuri saba.
2 Tena nikamwona malaika mwenye nguvu akitangaza kwa sauti kubwa:
“Nani anayestahili kuvunja hiyo mihuri na kukifungua kitabu hicho?”
3 Lakini hakupatikana mtu yeyote mbinguni, wala duniani, wala chini
Kuzimu, aliyeweza kukifungua hicho kitabu au kukitazama ndani.
4 Basi, mimi nikalia sana kwa sababu hakupatikana mtu aliyestahili
kukifungua, au kukitazama ndani.
5 Kisha mmoja wa wale wazee akaniambia, “Usilie! Tazama! Simba wa
kabila la Yuda, mjukuu maarufu wa Daudi, ameshinda. Yeye anaweza
kuivunja mihuri yake saba na kukifungua hicho kitabu.”
\fr 5:8
\f taz Zab 141:2
\fr 5:9
\f taz Zab 33:3; 98:1

6 Kisha nikaona pale katikati ya kiti cha enzi Mwana kondoo
amesimama, akizungukwa kila upande na vile viumbe hai vinne, na wale
wazee. Huyo Mwanakondoo alionekana kana kwamba amechinjwa. Alikuwa na
pembe saba na macho saba ambayo ni roho saba za Mungu zilizokuwa
zimepelekwa kila mahali duniani.
7 Mwanakondoo akaenda, akakitwaa hicho kitabu kutoka mkono wa kulia
wa yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi.
8 Mara tu alipokwisha twaa hicho kitabu, vile viumbe hai vinne
pamoja na wale wazee ishirini na wanne walianguka kifudifudi mbele ya
Mwanakondoo. Kila mmoja, alikuwa na kinubi na bakuli za dhahabu
zilizojaa ubani, ambao ni sala za watu wa Mungu.
9 Basi, wakaimba wimbo huu mpya:

“Wewe unastahili kukitwaa hicho kitabu
na kuivunja mihuri yake.
Kwa sababu wewe umechinjwa,
na kwa damu yako
umemnunulia Mungu watu
kutoka katika kila kabila, lugha, jamaa na taifa.

10 Wewe umewafanya wawe ufalme wa makuhani

wamtumikie Mungu wetu
nao watatawala duniani.”

11 Kisha nikatazama, nikasikia sauti ya malaika wengi sana, idadi
isiyohesabika, maelfu na maelfu. Walikuwa wamekaa kuzunguka kiti cha
enzi, vile viumbe hai vinne na wale wazee;
12 wakasema kwa sauti kuu:

“Mwanakondoo aliyechinjwa
anastahili kupokea uwezo, utajiri,
hekima, nguvu, utukufu na sifa.”
\m
13 Nikasikia viumbe vyote mbinguni, duniani, chini kuzimuni na
baharini–viumbe vyote ulimwenguni–vikisema: “Kwake yeye aketiye
katika kiti cha enzi, na kwa Mwanakondoo, iwe sifa na heshima na utukufu
na enzi milele na milele.”
14 Na vile viumbe vinne hai vikasema, “Amina!” Na wale wazee
wakaanguka kifudifudi, wakaabudu.

\c 6

Mwanakondoo anaivunja mihuri

1 Kisha nikamwona Mwanakondoo anavunja mhuri mmojawapo wa ile mihuri
saba. Nikasikia kimoja cha vile viumbe hai vinne kikisema kwa sauti kama
ya ngurumo, “Njoo!”
2 Mimi nikatazama, na kumbe palikuwa na farasi mmoja mweupe hapo. Na
mpanda farasi wake alikuwa na upinde, akapewa na taji. Basi, akatoka
kama mshindi aendelee kushinda.

3 Kisha, Mwanakondoo akavunja mhuri wa pili. Nikamsikia yule kiumbe
hai wa pili akisema, “Njoo!”
4 Nami nikatazama na kumbe palikuwapo farasi mwingine hapo,
mwekundu. Mpanda farasi wake alikabidhiwa jukumu la kuondoa amani
duniani, watu wauane, akapewa upanga mkubwa.

5 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tatu. Nikamsikia yule kiumbe
hai wa tatu akisema, “Njoo!” Nikatazama na kumbe palikuwapo farasi
mmoja hapo, mweusi. Mpanda farasi wake alikuwa na vipimo viwili vya
kupimia uzito mkononi mwake.
6 Nikasikia kitu kama sauti itokayo kwa vile viumbe hai vinne. Nayo
ilisema, “Kibaba kimoja cha unga wa ngano wa kiasi cha fedha dinari
moja, na vibaba vitatu vya shayiri kwa dinari moja. Lakini usiharibu
mafuta wala divai!”

7 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa nne. Nikamsikia yule kiumbe
hai wa nne akisema, “Njoo!”
8 Nami nikatazama, na kumbe alikuwapo farasi mmoja hapo, rangi yake
kijivu. Na jina la mpanda farasi wake lilikuwa kifo, na Kuzimu alimfuata
nyuma. Hao walipewa mamlaka juu ya robo moja ya dunia, wawaue watu kwa
upanga, njaa, tauni na kwa wanyama wakali wa dunia.

9 Kisha Mwanakondoo akavunja mhuri wa tano. Nikaona pale chini ya
madhabahu ya kufukizia ubani roho za wale waliouawa kwa sababu ya ujumbe
wa Mungu, na kwa sababu ya ushuhuda waliotoa.
10 Basi, wakalia kwa sauti kubwa: “Ee Bwana, uliye mtakatifu na
mwaminifu, mpaka lini utakawia kulipiza kisasi kwa wakazi wote wa dunia
kwa ajili ya kuuawa kwetu?”
11 Wakapewa kila mmoja vazi refu jeupe, wakaambiwa wazidi kusubiri
kwa muda mfupi, mpaka itakapotimia idadi ya watumishi wenzao na ndugu
ambao watawaua kama wao wenyewe walivyouawa.

12 Kisha nikatazama, na wakati Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa
sita, kukawa na tetemeko kubwa la ardhi; jua likawa jeusi kama gunia;
mwezi wote ukawa mwekundu kama damu;
13 nazo nyota za mbingu zikaanguka juu ya ardhi kama matunda ya
mtini yasiyokomaa yaangukavyo wakati mti wake unapotikiswa na upepo
mkali.
14 Anga likatoweka kama vile karatasi inavyokunjwakunjwa; milima
yote na visima vyote vikaondolewa mahali pake.
15 Kisha wafalme wa duniani, wakuu, majemadari, matajiri, wenye
nguvu, kila mtumwa na mtu huru, wakajificha mapangoni na kwenye majabali
milimani.
16 Wakaiambia hiyo milima na hayo majabali, “Tuangukieni,
mkatufiche mbali na yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na mbali na
ghadhabu ya Mwanakondoo!
17 Maana siku maalum ya ghadhabu yao imefika. Nani awezaye
kuikabili?”

\c 7

Kupigwa mhuri kwa watu 144,000 wa Israeli

1 Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne
za dunia wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: wala
katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti.
2 Kisha nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki
akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaaza sauti na kuwaambia hao
malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari,
3 “Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha
wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso.”
4 Kisha nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu mia moja
arobaini na nne elfu wa makabila yote ya watu wa Israeli.
5 Kabila la Yuda walikuwa watu kumi na mbili elfu; kabila la
Reubeni, kumi na mbili elfu, kabila la Gadi, kumi na mbili elfu;
6 Kabila la Asheri, kumi na mbili elfu; kabila la Naftali, kumi na
mbili elfu; kabila la Manase, kumi na mbili elfu;
7 kabila la Simeoni, kumi na mbili elfu, kabila la Lawi, kumi na
mbili elfu, kabila la Isakari, kumi na mbili elfu;
8 kabila la Zabuloni, kumi na mbili elfu; kabila la Yosefu, kumi na
mbili elfu, na kabila la Benyamini, kumi na mbili elfu.

Umati wa watu wa kila taifa

9 Kisha nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: watu
wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya
kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wakiwa wamevaa mavazi meupe na
kushika matawi ya mitende mikononi mwao.
10 Wakapaaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye
juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!”
11 Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na vile
viumbe hai vinne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi,
wakamwabudu Mungu,
12 wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima,
uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!”

13 Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni
watu gani? Na wametoka wapi?”
14 Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia,
“Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha
mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa.
15 Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia
Mungu mchana na usiku katika Hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha
enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda.
16 Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma
tena,
17 kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa
mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uzima. Naye
Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”

\c 8

Mhuri wa saba

1 Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa
muda wa nusu saa.
2 Kisha nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu
wamepewa tarumbeta saba.

3 Malaika mwingine akafika, akiwa anachukua chetezo cha dhahabu,
akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani
mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu, juu ya
madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi.
4 Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu,
kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.
5 Kisha malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa
madhabahuni akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na
tetemeko la ardhi.

Tarumbeta

6 Kisha wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari
kupiga mbiu ya mgambo.
\il 5
ic
\is Tarumbeta (Ufu. 8:6)
\ie

7 Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya
mawe na moto, pamoja na damu, ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya
nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua, na majani yote mabichi
yakaungua.

8 Malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa
unaowaka moto ukatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu,
9 theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa na theluthi moja ya
meli zikaharibiwa.

10 Kisha malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa
ikiwaka kama bonge la moto, ikaanguka kutoka mbinguni, na kutua juu ya
theluthi moja ya mito na chemchemi za maji.
11 (Nyota hiyo inaitwa “Uchungu.”) Basi, theluthi moja ya maji
yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu
yaligeuka kuwa machungu.

12 Kisha malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja
ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza
theluthi moja ya mng’ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga,
hali kadhalika na theluthi moja ya usiku.

13 Kisha nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani anasema
kwa sauti kubwa, “Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika
watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!”

\c 9

1 Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota
iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa
shimo la Kuzimu.
2 Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa
tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu.
3 Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu
kama ya ng’e.
4 Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti
yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika
paji la uso.
5 Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa
miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu
wakati anapoumwa na ng’e.
6 Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa
lakini kifo kitawakimbia.

7 Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari
kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na
nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.
8 Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa
kama meno ya simba.
9 Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya
mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi
wanaokimbilia vitani.
10 Walikuwa na mikia na miiba kama ng’e, na kwa mikia hiyo, walikuwa
na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano.
11 Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu;
jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani
mwangamizi.

12 Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.

13 Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia
sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa
mbele ya Mungu.
14 Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta,
“Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa <Eufrate!”>
15 Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa
wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka
huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu.
16 Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia
mbili.
17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo
njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya
samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya
simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao.
18 Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani,
moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao;
19 maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia
yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo
kuwadhuru watu.
\fr 9:20
\f taz Zab 115:4-7; 135:15-17

20 Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo,
hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao
wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba,
mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea.
21 Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na
wizi.

\c 10

Malaika na kitabu kidogo

1 Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka
mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu, na upinde wa mvua kichwani mwake. Uso
wake ulikuwa kama jua, na miguu yake ilikuwa kama moto.
2 Mikononi mwake alishika kitabu kidogo kimefunguliwa. Aliweka mguu
wake wa kulia juu ya bahari, na wa kushoto juu ya nchi kavu,
3 na kuita kwa sauti kubwa kama ya mngurumo wa simba. Alipopaaza
sauti, ngurumo saba ziliitikia kwa kishindo.
4 Na hizo ngurumo saba ziliposema, mimi nikataka kuandika. Lakini
nikasikia sauti kutoka mbinguni: “Maneno ya ngurumo hizo saba ni siri;
usiyaandike!”

5 Kisha yule malaika niliyemwona akisimama juu ya bahari na juu ya
nchi kavu akainua mkono wake wa kulia juu mbinguni,
6 akaapa kwa jina la Mungu aishiye milele na milele, Mungu aliyeumba
mbingu na vyote vilivyomo, bahari na vyote vilivyomo, dunia na vyote
vilivyomo. Akasema, “Wakati wa kusubiri zaidi umekwisha!
7 Lakini wakati ule malaika wa saba atakapotoa sauti yake, wakati
atakapopiga tarumbeta yake, Mungu atakamilisha mpango wake wa siri kama
alivyowatangazia watumishi wake manabii.”

8 Kisha ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni pale awali
ikasema nami tena: “Nenda ukakichukue kile kitabu kilichofunguliwa,
kilicho mkononi mwa malaika asimamaye juu ya bahari na juu ya nchi
kavu.”
9 Basi, nikamwendea huyo malaika, nikamwambia anipe hicho kitabu
kidogo. Naye akaniambia, “Kichukue, ukile; kinywani mwako kitakuwa
kitamu kama asali, lakini tumboni kitakuwa kichungu!”

10 Basi, nikakichukua kitabu hicho kidogo kutoka mkononi mwa huyo
malaika, nikakila; nacho kilikuwa kitamu kinywani mwangu kama asali,
lakini nilipokimeza kikawa kichungu tumboni mwangu.
11 Kisha nikaambiwa, “Inakubidi tena kutangaza ujumbe wa Mungu
kuhusu watu wengi, mataifa, watu wa lugha nyingi na wafalme!”

\c 11

Mashahidi wawili

1 Kisha nikapewa mwanzi uliokuwa kama kijiti cha kupimia, nikaambiwa,
“Inuka, ukalipime Hekalu la Mungu, madhabahu ya kufukizia ubani, na
ukawahesabu watu wanaoabudu ndani ya Hekalu.
2 Lakini uache ukumbi ulio nje ya Hekalu; usiupime, maana huo
umekabidhiwa watu wa mataifa mengine, ambao wataukanyanga mji Mtakatifu
kwa muda wa miezi arobaini na miwili.
3 Nami nitawatuma mashahidi wangu wawili ili watangaze ujumbe wa
Mungu kwa muda huo wa siku elfu moja mia mbili na sitini wakiwa wamevaa
mavazi ya magunia.”

4 Hao mashahidi wawili ni miti miwili ya Mizeituni na taa mbili
zinazosimama mbele ya Bwana wa dunia.
5 Kama mtu akijaribu kuwadhuru, moto hutoka kinywani mwao na
kuwaangamiza adui zao; na kila mtu atakayejaribu kuwadhuru atakufa namna
hiyo.
6 Hao wanayo mamlaka ya kufunga anga, mvua isinyeshe wakati
wanapotangaza ujumbe wa Mungu. Tena wanayo mamlaka ya kuzigeuza
chemchemi zote za maji ziwe damu, na ya kusababisha maafa ya kila namna
duniani kila mara wapendavyo.

7 Lakini wakisha maliza kutangaza ujumbe huo, mnyama atokaye shimoni
kuzimu atapigana nao, atawashinda na kuwaua.
8 Maiti zao zitabaki katika barabara za mji mkuu ambapo Bwana wao
alisulubiwa; jina la kupanga la mji huo ni Sodoma au Misri.
9 Watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti
hizo kwa muda wa siku tatu na nusu, na hawataruhusu zizikwe.
10 Watu waishio duniani watafurahia kifo cha hao wawili. Watafanya
sherehe na kupelekeana zawadi maana manabii hawa wawili walikuwa
wamewasumbua mno watu wa dunia.
11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu pumzi ya uhai kutoka kwa
Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu
kuu.
12 Kisha hao manabii wawili wakasikia sauti kubwa kutoka mbinguni
ikiwaambia, “Njoni hapa juu!” Nao wakapanda juu mbinguni katika wingu,
maadui wao wakiwa wanawatazama.
13 Wakati huohuo, kukatokea tetemeko kubwa la ardhi, sehemu moja ya
kumi ya ardhi ikaharibiwa. Watu elfu saba wakauawa kwa tetemeko hilo la
ardhi. Watu waliosalia wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.
14 Maafa ya pili yamepita; lakini tazama! Maafa ya tatu yanafuata
hima.

Tarumbeta ya saba

15 Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu
zikasikika mbinguni zikisema, “Sasa utawala juu ya ulimwengu ni wa
Bwana wetu na Kristo wake. Naye atatawala milele na milele!”
16 Kisha wale wazee ishirini na wanne walioketi mbele ya Mungu
katika viti vyao vya enzi, wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu,
17 wakisema:

“Bwana Mungu Mwenye uwezo,
uliyeko na uliyekuwako!
Tunakushukuru,
maana umetumia nguvu yako kuu ukaanza kutawala!

18 Watu wa mataifa waliwaka hasira,

maana wakati wa ghadhabu yako umefika,
wakati wa kuwahukumu wafu.
Ndio wakati wa kuwatuza
watumishi wako manabii,
watu wako na wote wanaolitukuza
jina lako, wakubwa kwa wadogo.
Ni wakati wa kuwaangamiza
wale wanaoangamiza dunia.”
\fr 11:18
\f taz Zab 2:5; 110:5; 115:13

19 Hekalu la Mungu mbinguni likafunguliwa, na Sanduku la Agano lake
likaonekana Hekaluni mwake. Kisha kukatokea umeme, sauti, ngurumo,
tetemeko la ardhi, na mvua kubwa ya mawe.

\c 12

Mwanamke na joka

1 Kisha ishara kubwa ikaonekana mbinguni. Palikuwa hapo mwanamke
aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na
mbili juu ya kichwa chake!
2 Alikuwa mja mzito, na akapaaza sauti kwa maumivu na uchungu wa
kujifungua mtoto.
\fr 12:5
\f taz Zab 2:9

3 Ishara nyingine ikatokea mbinguni: joka kubwa jekundu na lenye
pembe kumi na vichwa saba; na kila kichwa kilikuwa na taji.
4 Joka hilo liliburuta kwa mkia wake theluthi moja ya nyota za anga
na kuzitupa duniani. Nalo lilisimama mbele ya huyo mama aliyekuwa karibu
kujifungua mtoto, tayari kabisa kummeza mtoto, mara tu atakapozaliwa.
5 Kisha mama huyo akajifungua mtoto wa kiume, ambaye atayatawala
mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Lakini mtoto akanyakuliwa na kupelekwa
kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi.
6 Huyo mama akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa
amemtayarishia mahali pa usalama ambapo angehifadhiwa kwa muda wa siku
elfu moja mia mbili na sitini.

7 Kisha kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana
na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake.
8 Lakini joka hilo halikuweza kuwashinda, na hatimaye hapakuwa tena
na nafasi mbinguni kwa ajili yake na malaika wake.
9 Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa
kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani. Ndiye anayeudanganya
ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja
naye.

10 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: “Sasa
ukombozi utokao kwa Mungu umefika! Nguvu na Utawala wa Mungu wetu
umedhihirika. Na Kristo wake ameonyesha mamlaka yake! Maana yule
mdhalimu wa ndugu zetu, aliyesimama mbele ya Mungu akiwashtaki usiku na
mchana, sasa ametupwa nje.
11 Ndugu zetu wameshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa nguvu ya
ukweli walioutangaza; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana,
wakawa tayari kufa.
12 Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani
yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na
ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba siku zake zilizobakia ni
chache.”

13 Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza
kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume.
14 Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali
sana na hilo joka, mpaka mahali, pake jangwani ambapo angehifadhiwa
salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu.
15 Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama
nyuma ili yamchukue.
16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: ikajifunua kama mdomo na
kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka.
17 Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda
kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za
Mungu na kuuzingatia ukweli wa Yesu.
18 Na likajisimamia ukingoni mwa bahari.

\c 13

Wanyama wawili

1 Kisha nikaona mnyama mmoja akitoka baharini. Alikuwa na vichwa saba
na pembe kumi, na kila pembe ilikuwa na taji. Jina la kashfa lilikuwa
limeandikwa juu ya vichwa hivyo.
2 Mnyama huyo niliyemwona alikuwa kama chui; miguu yake ilikuwa kama
ya dubu, na kinywa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama
nguvu yake, kiti chake cha enzi na uwezo mkuu.
3 Kichwa kimojawapo cha huyo mnyama kilionekana kama kilikwisha
jeruhiwa vibaya sana, lakini jeraha hilo lilikuwa limepona. Dunia nzima
ilishangazwa na huyo mnyama na kumfuata.
4 Watu wote wakaliabudu lile joka kwa sababu lilimpa huyo mnyama
uwezo wake. Wakamwabudu pia huyo mnyama wakisema, “Nani aliye kama huyu
mnyama? Ni nani awezaye kupigana naye?”

5 Kisha huyo mnyama akaruhusiwa kusema maneno ya kujigamba na
kumkufuru Mungu; akaruhusiwa kuwa na mamlaka kwa muda wa miezi arobaini
na miwili.
6 Basi, akaanza kumtukana Mungu, kulitukana jina lake, makao yake,
na wote wakaao mbinguni.
7 Aliruhusiwa kuwapiga vita na kuwashinda watu wa Mungu. Alipewa
mamlaka juu ya watu wa kila kabila, ukoo, lugha na taifa.
8 Wote waishio duniani watamwabudu isipokuwa tu wale ambao majina
yao yameandikwa tangu mwanzo wa ulimwengu katika kitabu cha uzima cha
Mwanakondoo aliyechinjwa.
\fr 13:8
\f taz Zab 69:28

9 “Aliye na masikio, na asikie!
10 Waliokusudiwa kuchukuliwa mateka lazima watatekwa; waliokusudiwa
kuuawa kwa upanga lazima watauawa kwa upanga. Kutokana na hayo ni lazima
watu wa Mungu wawe na uvumilivu na imani.”

11 Kisha nikamwona mnyama mwingine anatoka ardhini. Alikuwa na pembe
mbili kama pembe za kondoo, na aliongea kama joka.
12 Alikuwa na mamlaka kamili kutoka kwa yule mnyama wa kwanza, na
akautumia uwezo huo mbele ya huyo mnyama. Akailazimisha dunia yote na
wote waliomo humo kumwabudu huyo mnyama wa kwanza ambaye alikuwa na
jeraha la kifo lililokuwa limepona.
13 Basi, huyu mnyama wa pili akafanya miujiza mikubwa hata
akasababisha moto kutoka mbinguni ushuke duniani mbele ya watu.
14 Aliwapotosha wakazi wa dunia kwa miujiza hiyo aliyojaliwa kutenda
mbele ya mnyama wa kwanza. Aliwaambia wakazi wa dunia watengeneze sanamu
kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini
akaishi tena.
15 Kisha alijaliwa kuipulizia uhai hiyo sanamu ya yule mnyama wa
kwanza, hata ikaweza kuongea na kuwaua watu wote ambao hawakuiabudu.
16 Aliwalazimisha wote, wadogo na wakubwa, matajiri na maskini, watu
huru na watumwa, watiwe alama juu ya mikono yao ya kulia au juu ya paji
za nyuso zao.
17 Akapiga marufuku mtu yeyote kununua au kuuza kitu isipokuwa tu
mtu aliyetiwa alama hiyo, yaani jina la yule mnyama au tarakimu ya jina
hilo.

18 Hapa ni lazima kutumia ujasiri! Mwenye akili anaweza kufafanua
maana ya tarakimu ya mnyama huyo, maana ni tarakimu yenye maana ya mtu
fulani. Tarakimu hiyo ni mia sita sitini na sita.

\c 14

Wimbo wa watu waliokombolewa

1 Kisha nikaona mlima Sioni, na Mwanakondoo amesimama juu yake;
pamoja naye walikuwa watu mia moja arobaini na nne elfu ambao juu ya
paji za nyuso zao walikuwa wameandikwa jina la Mwanakondoo na jina la
Baba yake.
2 Basi, nikasikia sauti kutoka mbinguni, sauti iliyokuwa kama sauti
ya maji mengi na kama sauti ya ngurumo kubwa. Sauti niliyosikia ilikuwa
kama sauti ya wachezaji muziki wakipiga vinubi vyao.
3 Walikuwa wanaimba wimbo mpya mbele ya kiti cha enzi na mbele ya
wale viumbe hai wanne na wale wazee. Hakuna mtu aliyeweza kujifunza
wimbo huo isipokuwa hao watu mia moja arobaini na nne elfu
waliokombolewa duniani.
4 Watu hao ndio wale waliojiweka safi kwa kutoonana kimwili na
wanawake, nao ni mabikira. Wao humfuata Mwanakondoo kokote aendako.
Wamekombolewa kutoka miongoni mwa binadamu wengine, wakawa wa kwanza
kutolewa kwa Mungu na kwa Mwanakondoo.
5 Hawakupata kamwe kuwa waongo; hawana hatia yoyote.

Malaika wa tatu

6 Kisha nikamwona malaika mwingine anaruka juu angani akiwa na
Habari Njema ya milele ya Mungu, aitangaze kwa watu wote waishio
duniani, kwa mataifa yote, makabila yote, watu wa lugha zote na rangi
zote.
7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumtukuza! Maana saa
imefika ya kutoa hukumu yake. Mwabuduni yeye aliyeumba mbingu na nchi,
bahari na chemchemi za maji.”

8 Malaika wa pili alimfuata huyo wa kwanza akisema, “Ameanguka!
Naam, Babuloni mkuu ameanguka! Babuloni ambaye aliwapa mataifa yote
wainywe divai yake–divai kali ya uzinzi wake!”

9 Na malaika wa tatu aliwafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa,
“Yeyote anayemwabudu yule mnyama na sanamu yake na kukubali kutiwa
alama yake juu ya paji la uso wake au juu ya mkono wake,
10 yeye mwenyewe atakunywa divai ya ghadhabu ya Mungu, ambayo
imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake bila kuchanganywa na maji.
Mtu huyo atateseka ndani ya moto na kiberiti mbele ya malaika watakatifu
na mbele ya Mwanakondoo.
11 Moshi wa moto unaowatesa kupanda juu milele na milele. Watu hao
waliomwabudu huyo mnyama na sanamu yake, na kutiwa alama ya jina lake,
hawatakuwa na nafuu yoyote usiku na mchana.”

12 Kutokana na hayo, ni lazima watu wa Mungu, yaani watu wanaotii
amri ya Mungu na kumwamini Yesu, wawe na uvumilivu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika! Heri
watu ambao tangu sasa wanakufa wakiwa wameungana na Bwana.” Naye Roho
asema, “Naam! Watapumzika kutoka taabu zao; maana matunda ya jasho lao
yatawafuata.”

14 Kisha nikatazama, na kumbe palikuwapo wingu jeupe hapo. Na juu ya
wingu hilo kulikuwa na kiumbe kama mtu. Alikuwa amevaa taji ya dhahabu
kichwani, na kushika mundu mkononi mwake.
15 Kisha malaika mwingine akatoka Hekaluni, na kwa sauti kubwa
akamwambia yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu, “Tafadhali, tumia mundu
wako ukavune mavuno, maana wakati wa mavuno umefika; mavuno ya dunia
yameiva.”
16 Basi, yule aliyekuwa amekaa juu ya wingu akautupa mundu wake
duniani, na mavuno ya dunia yakavunwa.
17 Kisha malaika mwingine akatoka katika Hekalu mbinguni akiwa na
mundu wenye makali.

18 Kisha malaika mwingine msimamizi wa moto, akatoka madhabahuni
akamwambia kwa sauti kubwa yule malaika mwenye mundu wenye makali,
“Nawe tia huo mundu wako mkali, ukakate vichala vya mizabibu ya dunia,
maana zabibu zake zimeiva!”
19 Basi, malaika huyo akautupa mundu wake duniani, akakata zabibu za
dunia, akazitia ndani ya chombo kikubwa cha kukamulia zabibu, chombo cha
ghadhabu ya Mungu.
20 Zabibu zikakamuliwa ndani ya hilo shinikizo lililoko nje ya mji,
na damu ikatoka katika shinikizo hilo mtiririko mrefu kiasi cha mita mia
tatu na kina chake kiasi cha mita mia mbili.

\c 15

Misiba mikuu ya mwisho

1 Kisha nikaona ishara nyingine mbinguni, kubwa na ya kushangaza.
Palikuwa hapo malaika saba wenye mabaa makubwa saba ya mwisho. Kwa mabaa
hayo makubwa saba, ghadhabu ya Mungu imekamilishwa.
2 Kisha nikaona kitu kama bahari ya kioo, imechanganywa na moto.
Nikawaona pia wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake na
ambaye jina lake lilitajwa kwa ile tarakimu. Watu hao walikuwa
wamesimama kando ya hiyo bahari ya kioo, wakiwa na vinubi walivyopewa na
Mungu.
3 Walikuwa wakiimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu, na wimbo wa
Mwanakondoo:

“Bwana Mungu Mwenye Uwezo,
matendo yako ni makuu mno!
Ewe Mfalme wa mataifa,
njia zako ni za haki na za kweli!

4 Bwana, ni nani asiyekucha wewe?

Nani asiyelitukuza jina lako?
Wewe peke yako ni Mtakatifu.
Mataifa yote yatakujia na kukuabudu
maana matendo yako ya haki yameonekana na wote.”
\fr 15:4
\f taz Zab 86:9

5 Baada ya hayo nikaona Hekalu limefunguliwa mbinguni, na ndani yake
hema ionyeshayo kuwapo kwa Mungu.
6 Basi, wale malaika saba wenye mabaa saba wakatoka humo Hekaluni,
wakiwa wamevaa nguo za kitani safi zenye kung’aa, na kanda za dhahabu
vifuani mwao.
7 Kisha, mmojawapo wa vile viumbe vinne akawapa hao malaika saba
mabakuli ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, aishiye milele na
milele.
8 Hekalu likajaa moshi uliosababishwa na utukufu na nguvu ya Mungu,
na hakuna mtu aliyeweza kuingia Hekaluni mpaka mwisho wa mabaa makubwa
saba ya wale malaika saba.

\c 16

Mabakuli ya ghadhabu ya Mungu

1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka Hekaluni ikiwaambia wale malaika
saba, “Nendeni mkamwage mabakuli hayo saba ya ghadhabu ya Mungu
duniani.”

2 Basi, malaika wa kwanza akaenda akamwaga bakuli lake juu ya nchi.
Mara madonda mabaya na ya kuumiza sana yakawapata wote waliokuwa na
alama ya yule mnyama, na wale walioiabudu sanamu yake.

3 Kisha malaika wa pili akamwaga bakuli lake baharini. Nayo bahari
ikawa damu tupu kama damu ya mtu aliyekufa, na viumbe vyote hai baharini
vikafa.
\fr 16:4
\f taz Zab 78:44

4 Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za
maji, navyo vikageuka damu.
5 Nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema,

“Ewe mtakatifu,
Uliyeko na uliyekuwako!
Wewe ni mwenye haki katika hukumu hii uliyotoa.

6 Maana waliimwaga damu ya watu wako na ya manabii,

nawe umewapa damu wainywe;
wamestahili hivyo!”
\m
7 Kisha nikasikia sauti madhabahuni ikisema, “Naam, Bwana Mungu
Mwenye Uwezo! Hukumu zako ni za kweli na haki!”

8 Kisha malaika wa nne akamwaga bakuli lake juu ya jua. Jua likapewa
nguvu ya kuwachoma watu kwa moto wake.
9 Basi, watu wakaunguzwa vibaya sana; wakamtukana Mungu aliye na
uwezo juu ya mabaa hayo makubwa. Lakini hawakuziacha dhambi zao na
kumtukuza Mungu.

10 Kisha malaika wa tano akamwaga bakuli lake juu ya makao makuu ya
yule mnyama. Giza likauvamia utawala wake, watu wakauma ndimi zao kwa
sababu za maumivu,
11 wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na
madonda yao. Lakini hawakuyaacha matendo yao mabaya.

12 Kisha malaika wa sita akamwaga bakuli lake juu ya mto mkubwa
uitwao Eufrate. Maji yake yakakauka, na hivyo njia ilitengenezwa kwa
ajili ya wafalme wa mashariki.
13 Kisha nikaona pepo wabaya watatu walio kama vyura, wakitoka
kinywani mwa yule joka, kinywani mwa yule mnyama, na kinywani mwa yule
nabii wa uongo.
14 Hawa ndio roho za pepo wafanyao miujiza. Ndio wanaokwenda kwa
wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya pamoja kwa ajili ya vita kuu
Siku ile ya Mungu Mwenye Uwezo.

15 “Sikiliza! Mimi naja kama mwizi! Heri mtu akeshaye na kuvaa nguo
zake ili asije akaenda uchi huko na huko mbele ya watu.”

16 Basi, roho hao wakawakusanya hao wafalme mahali paitwapo kwa
Kiebrania Harmagedoni.

17 Kisha malaika wa saba akamwaga bakuli lake hewani. Sauti kubwa
ikasikika kutoka kwenye kiti cha enzi, Hekaluni, ikisema, “Mwisho
umefika!”
18 Kukatokea umeme, kelele, ngurumo na tetemeko kubwa la ardhi
ambalo halijapata kutokea tangu Mungu alipomuumba mtu.
19 Mji ule mkuu ukapasuliwa sehemu tatu, nayo miji ya mataifa
ikateketea. Babuloni, mji mkuu, haukusahauliwa na Mungu. Aliunywesha
kikombe cha divai ya ghadhabu yake kuu.
20 Visiwa vyote vikatoweka, nayo milima haikuonekena tena.
21 Mvua ya mawe makubwa yenye uzito wa kama kilo hamsini kila moja,
ikawanyeshea watu. Nao wakamtukana Mungu kwa sababu ya mapigo ya mvua
hiyo ya mawe. Naam, pigo la mvua hiyo ya mawe lilikuwa kubwa mno.

\c 17

Mzinzi mkuu

1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na bakuli akaja, akaniambia,
“Njoo, mimi nitakuonyesha adhabu aliyopewa yule mzinzi mkuu, mji ule
uliojengwa juu ya maji mengi.
2 Wafalme wa dunia wamefanya uzinzi pamoja naye; na wakazi wa dunia
wamelewa divai ya uzinzi wake.”

3 Kisha, Roho akanikumba, akaniongoza mpaka jangwani. Huko nikamwona
mwanamke ameketi juu ya mnyama mwekundu. Mnyama huyo alikuwa ameandikwa
kila mahali majina ya makufuru; alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.
4 Mwanamke huyo alikuwa amevaa vazi la rangi ya zambarau na
nyekundu; alikuwa amejipamba kwa dhahabu, mawe ya thamani na lulu.
Mkononi mwake alishika kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa
machukizo na mambo machafu yanayoonyesha uzinzi wake.
5 Alikuwa ameandikwa juu ya paji la uso wake jina la fumbo
“Babuloni mkuu, mama wa wazinzi na wa mambo yote ya kuchukiza sana
duniani.”
6 Nikamwona huyo mwanamke amelewa damu ya watu wa Mungu, na damu ya
watu waliouawa kwa sababu ya kumtangaza Yesu.
Nilipomwona nilishangaa mno.
7 Lakini malaika akaniambia, “Kwa nini unashangaa? Mimi nitakuambia
maana iliyofichika ya mwanamke huyu na mnyama huyo amchukuaye ambaye ana
vichwa saba na pembe kumi.
8 Huyo mnyama uliyemwona alikuwa hai hapo awali, lakini sasa
amekufa. Hata hivyo, karibu sana atapanda kutoka shimoni kuzimu, lakini
ataangamizwa. Wanaoishi duniani watashangaa; naam, watu wote ambao
majina yao hayakupata kuandikwa katika kitabu cha uzima tangu mwanzo wa
ulimwengu, watashangaa kumwona huyo mnyama ambaye hapo awali, aliishi,
kisha akafa na sasa anatokea tena!
\fr 17:8
\f taz Zab 69:28

9 “Hapa panahitaji akili na hekima! Hivyo vichwa saba ni vilima
saba, na huyo mwanamke anaketi juu yake. Vichwa hivyo pia ni wafalme
saba.
10 Kati ya hao wafalme saba, watano wamekwisha angamia, mmoja
anatawala bado, na yule mwingine bado hajafika; na atakapofika atabaki
kwa muda mfupi.
11 Huyo mnyama ambaye alikuwa anaishi hapo awali lakini sasa haishi
tena ni mfalme wa nane, naye pia ni miongoni mwa hao saba, na anakwenda
zake kuharibiwa.

12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme ambao bado hawajaanza
kutawala. Lakini watapewa mamlaka ya kutawala kwa muda wa saa moja
pamoja na yule mnyama.
13 Shabaha ya hawa kumi ni moja, na watampa yule mnyama nguvu na
mamlaka yao yote.
14 Watapigana na Mwanakondoo, lakini Mwanakondoo pamoja na wale
aliowaita na kuwachagua, ambao ni waaminifu, atawashinda kwa sababu yeye
ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme.”

15 Malaika akaniambia pia, “Yale maji uliyoyaona pale alipokaa yule
mzinzi, ni mataifa, watu wa kila rangi na lugha.
16 Pembe zile kumi ulizoziona na yule mnyama watamchukia huyo
mzinzi. Watachukua kila kitu alicho nacho na kumwacha uchi; watakula
nyama yake na kumteketeza kwa moto.
17 Maana Mungu ametia mioyoni mwao nia ya kutekeleza shabaha yake,
yaani kwa kukubaliana wao kwa wao na kumpa huyo mnyama mamlaka yao ya
kutawala, mpaka hapo neno la Mungu litakapotimia.

18 “Na yule mwanamke uliyemwona ndio ule mji mkuu unaowatawala
wafalme wa dunia.”

\c 18

Kuangamia kwa Babuloni

1 Baada ya hayo, nilimwona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni.
Alikuwa na uwezo mkuu, na dunia ikamulikwa na mng’ao wake.
2 Basi, akapaaza sauti kwa nguvu akisema, “Umeanguka; Babuloni mkuu
umeanguka! Sasa umekuwa makao ya mashetani na pepo wachafu; umekuwa
makao ya ndege wachafu na wa kuchukiza mno.
3 Maana mataifa yote yalileweshwa kwa divai kali ya uzinzi wake, nao
wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye. Nao wafanyabiashara wa dunia
wametajirika kutokana na anasa zake zisizo na kipimo.”

4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema,
“Watu wangu, ondokeni kwake, ili msishirikiane naye katika dhambi
zake, msije mkaipata adhabu yake.
5 Kwa maana dhambi zake zimekuwa nyingi mno, zimelundikana mpaka
mbinguni, na Mungu ameyakumbuka maovu yake.
6 Mtendeeni kama alivyowatendea ninyi; mlipeni mara mbili kwa yale
aliyoyatenda. Jazeni kikombe chake kwa kinywaji kikali mara mbili zaidi
ya kile alichowapeni.
7 Mpeni mateso na uchungu kadiri ya kujigamba kwake, na kuishi kwake
kwa anasa. Maana anajisemea moyoni: <Ninaketi hapa; mimi ni malkia. Mimi
si mjane, wala sitapatwa na uchungu!>
8 Kwa sababu hiyo mabaa yake yatampata kwa siku moja: ugonjwa,
huzuni na njaa. Atachomwa moto, maana Bwana Mungu mwenye kumhukumu ni
Mwenye Uwezo.”
\fr 18:6
\f taz Zab 137:8

9 Wafalme wa Dunia waliofanya uzinzi naye na kuishi naye maisha ya
anasa wataomboleza na kulia wakati watakapoona moshi wa mji huo
unaoteketea.
10 Wanasimama kwa mbali kwa sababu ya kuogopa mateso yake, na
kusema, “Ole! Ole kwako Babuloni, mji maarufu na wenye nguvu! Kwa muda
wa saa moja tu adhabu yako imekupata.”

11 Wafanyabiashara wa dunia watalia na kumfanyia matanga, maana
hakuna mtu anayenunua tena bidhaa zao;
12 hakuna tena wa kununua dhahabu yao, fedha, mawe ya thamani na
lulu, kitani na nguo za rangi ya zambarau, hariri na nguo nyekundu;
vyombo vya kila aina ya miti ya pekee, vyombo vya pembe za ndovu, vya
miti ya thamani kubwa, vya shaba, chuma na marmari;
13 mdalasini, viungo, ubani, manemane, udi, divai, mafuta, unga na
ngano, ng’ombe na kondoo, farasi na magari ya kukokotwa, watumwa wao na
hata maisha ya watu.
14 Wafanyabiashara wanamwambia: “Faida yote uliyotazamia imetoweka,
na utajiri na fahari vimekuponyoka; hutaweza kuvipata tena!”
15 Wafanya biashara waliotajirika kutokana na mji huo, watasimama
mbali kwa sababu ya hofu ya mateso yake, watalalamika na kuomboleza,
16 wakisema, “Ole! Ole kwa mji huu mkuu. Ulizoea kuvalia nguo za
kitani, za rangi ya zambarau na nyekundu, na kujipamba kwa dhahabu, mawe
ya thamani na lulu!
17 Kwa saa moja tu utajiri wako umetoweka!”
Halafu manahodha wote na wasafiri wao, wanamaji na wote wanaofanya
kazi baharini, walisimama kwa mbali,
18 na walipouona moshi wa moto ule uliouteketeza, wakalia kwa sauti:
“Hakujapata kuwako mji kama mji huu mkuu!”
19 Wakajimwagia vumbi juu ya vichwa vyao wakilia kwa sauti na
kuomboleza: “Ole! Ole kwako mji mkuu! Ni mji ambamo wote wenye meli
zisafirizo baharini walitajirika kutokana na utajiri wake. Kwa muda wa
saa moja tu umepoteza kila kitu!”

20 Furahi ee mbingu, kwa sababu ya uharibifu wake. Furahini watu wa
Mungu, mitume na manabii! Kwa maana Mungu ameuhukumu kwa sababu ya mambo
uliyowatenda ninyi!

21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu sana akainua jiwe mfano wa jiwe
kubwa la kusagia, akalitupa baharini akisema, “Ndivyo, Babuloni
atakavyotupwa na kupotea kabisa.
22 Sauti za vinubi za muziki, sauti za wapiga filimbi na tarumbeta
hazitasikika tena ndani yako. Hakuna fundi wa namna yoyote ile
atakayepatikana tena ndani yako; wala sauti ya jiwe la kusagia
haitasikika tena ndani yako.
23 Mwanga wa taa hautaonekana tena ndani yako; sauti za bwana arusi
na bibi arusi hazitasikika tena ndani yako. Wafanyabiashara wako
walikuwa wakuu duniani, na kwa uchawi wako mataifa yote yalipotoshwa!”

24 Mji huo uliadhibiwa kwani humo mlipatikana damu ya manabii, damu
ya watu wa Mungu na damu ya watu wote waliouawa duniani.

\c 19

1 Baada ya hayo nikasikia kitu kama sauti kubwa ya umati wa watu
wengi mbinguni ikisema, “Haleluya! Ukombozi, utukufu na nguvu ni mali
yake Mungu wetu!
2 Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki. Amemhukumu yule mzinzi
mkuu ambaye alikuwa ameipotosha dunia kwa uzinzi wake. Amemwadhibu kwa
sababu ya kumwaga damu ya watumishi wake!”
3 Wakasema, “Asifiwe Mungu! Moshi wa moto unaoteketeza mji huo
utapanda juu milele na milele!”
4 Na wale wazee ishirini na wanne, na vile viumbe hai vinne,
wakajitupa chini, wakamwabudu Mungu aliyeketi juu ya kiti cha enzi
wakisema, “Amina! Asifiwe Mungu!”
\fr 19:5
\f taz Zab 115:13
\fr 19:6
\f taz Zab 93:1; 97:1; 99:1

Karamu ya arusi ya Mwanakondoo

5 Kisha kukatokea sauti kwenye kiti cha enzi: “Msifuni Mungu enyi
watumishi wake wote, nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.”
6 Kisha nikasikia kitu kama sauti ya umati mkubwa wa watu na sauti
ya maji mengi na ya ngurumo kubwa, ikisema, “Haleluya! Maana Bwana
Mungu wetu Mwenye Uwezo ni Mfalme!
7 Tufurahi na kushangilia; tumtukuze, kwani wakati wa arusi ya
Mwanakondoo umefika, na bibi arusi yuko tayari.
8 Amepewa uwezo wa kujivalia nguo ya kitani safi, iliyotakata na
yenye kung’aa!” (Nguo hiyo ya kitani safi ni matendo mema ya watu wa
Mungu.)

9 Kisha malaika akaniambia, “Andika haya: Heri wale walioalikwa
kwenye karamu ya arusi ya Mwanakondoo!” Tena akaniambia, “Hayo ni
maneno ya kweli ya Mungu.”
10 Basi, mimi nikaanguka kifudifudi mbele ya miguu yake nikataka
kumwabudu. Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe
na ndugu zako; sote tunauzingatia ukweli ule alioufunua Yesu. Mwabudu
Mungu! Maana ukweli alioufunua Yesu ndio unaowaangazia manabii.”
\fr 19:11
\f taz Zab 96:13

Farasi mweupe na mpanda farasi

11 Kisha nikaona mbingu zimefunguliwa; na huko alikuwako farasi
mmoja mweupe, na mpanda farasi wake aliitwa “Mwaminifu” na “Kweli”.
Huyo huhukumu na kupigana kwa ajili ya haki.
12 Macho yake ni kama mwali wa moto, na alikuwa amevaa taji nyingi
kichwani. Alikuwa ameandikwa jina ambalo hakuna mtu alijuaye isipokuwa
tu yeye mwenyewe.
13 Alikuwa amevaa vazi lililokuwa limelowekwa katika damu. Na jina
lake huyo ni “Neno la Mungu.”
14 Majeshi ya mbinguni yalimfuata yakiwa yamepanda farasi weupe na
walikuwa wamevaa mavazi ya kitani, meupe na safi.
15 Upanga mkali hutoka kinywani mwake, na kwa upanga huo atawashinda
mataifa. Yeye ndiye atakayetawala kwa fimbo ya chuma na kuikamua divai
katika chombo cha kukamulia zabibu za ghadhabu kuu ya Mungu Mwenye
Uwezo.
16 Juu ya vazi lake, na juu ya mguu wake, alikuwa ameandikwa jina:
“Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana.”
\fr 19:15
\f taz Zab 2:9

17 Kisha nikamwona malaika mmoja amesimama katika jua. Akapaaza
sauti na kuwaambia ndege wote waliokuwa wanaruka juu angani, “Njoni!
Kusanyikeni pamoja kwa karamu kuu ya Mungu.
18 Njoni mkaitafune miili ya wafalme, ya majemadari, ya watu wenye
nguvu, ya farasi na wapanda farasi wao; njoni mkaitafune miili ya watu
wote: walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

19 Kisha nikaona yule mnyama pamoja na mfalme wa dunia na askari wao
wamekusanyika pamoja kusudi wapigane na yule aliyekuwa ameketi juu ya
farasi, pamoja na jeshi lake.
20 Lakini huyo mnyama akachukuliwa mateka, pamoja na nabii wa uongo
aliyekuwa akifanya miujiza mbele yake. (Kwa miujiza hiyo, alikuwa
amewapotosha wale waliokuwa na chapa ya huyo mnyama, na ambao walikuwa
wameiabudu sanamu yake.) Huyo mnyama pamoja na huyo nabii walitupwa wote
wawili, wakiwa wazimawazima, ndani ya ziwa linalowaka moto wa kiberiti.
21 Majeshi yao yaliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule
anayepanda farasi. Ndege wote wakajishibisha kwa nyama zao.

\c 20

Miaka elfu moja

1 Kisha nikamwona malaika mmoja anashuka kutoka mbinguni akiwa na
ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake.
2 Akalikamata lile joka–nyoka wa kale, yaani Ibilisi au
Shetani–akalifunga kwa muda wa miaka elfu moja.
3 Malaika akalitupa Kuzimu, akaufunga mlango wa kuingilia huko na
kuutia mhuri ili lisiweze tena kuyapotosha mataifa mpaka hapo miaka elfu
moja itakapotimia. Lakini baada ya miaka hiyo ni lazima lifunguliwe
tena, lakini kwa muda mfupi tu.

4 Kisha nikaona viti vya enzi na watu walioketi juu yake; watu hao
walipewa mamlaka ya hukumu. Niliona pia roho za wale waliokuwa
wamenyongwa kwa sababu ya kumtangaza Yesu na kwa sababu ya neno la
Mungu. Hawa hawakumwabudu yule mnyama na sanamu yake, wala hawakupigwa
alama yake juu ya paji za nyuso zao, au juu ya mikono yao. Walipata tena
uhai, wakatawala pamoja na Kristo kwa muda wa miaka elfu moja.
5 (Wale wengine waliokufa hawakupata uhai mpaka miaka elfu moja
itimie.) Huu ndio ufufuo wa kwanza.
6 Wameneemeka sana, tena heri yao wote wanaoshiriki ufufuo huu wa
kwanza. Kifo cha pili hakitakuwa na nguvu juu yao; watakuwa makuhani wa
Mungu na wa Kristo, na watatawala pamoja naye kwa miaka elfu moja.

Kuangamizwa kwa Shetani

7 Wakati miaka elfu mia moja itakapotimia, Shetani atafunguliwa
kutoka gerezani mwake.
8 Basi, atatoka nje, ataanza kuyapotosha mataifa yote
yaliyotawanyika kila mahali duniani, yaani Gogu na Magogu. Shetani
atawakusanya pamoja kwa ajili ya vita; nao watakuwa wengi kama mchanga
wa pwani.
9 Walitawanyika katika nchi yote, wakaizunguka kambi ya watu wa
Mungu na mji wa Mungu aupendao. Lakini moto ulishuka kutoka mbinguni,
ukawaangamiza.
10 Ibilisi, aliyekuwa anawapotosha, akatupwa ndani ya ziwa
linalowaka moto wa kiberiti, walimo yule mnyama na yule nabii wa uongo,
nao watateswa mchana na usiku, milele na milele.

Hukumu ya mwisho

11 Kisha nikaona kiti cha enzi kikubwa cheupe, na yule aketiye juu
yake. Dunia na mbingu vikatoweka mbele ya macho yake, na havikuonekana
tena.
12 Kisha nikawaona watu wakubwa na wadogo, wamesimama mbele ya kiti
cha enzi, na vitabu vikafunguliwa. Halafu kitabu kingine, yaani kitabu
cha uzima, kikafunguliwa pia. Wafu wakahukumiwa kadiri ya matendo yao,
kama ilivyoandikwa ndani ya vitabu hivyo.
13 Bahari ikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yake; kifo na kuzimu
vikawatoa nje wafu waliokuwa ndani yao. Kila mmoja akahukumiwa kufuatana
na matendo yake.
14 Kisha kifo na kuzimu vikatupwa ndani ya ziwa la moto. Ziwa hili
la moto ndicho kifo cha pili.
15 Mtu yeyote ambaye jina lake halikupatikana limeandikwa katika
kitabu cha uzima, alitupwa katika ziwa la moto.

\c 21

Mbingu mpya na dunia mpya

1 Kisha nikaona mbingu mpya na dunia mpya. Mbingu ile ya kwanza na
dunia ile ya kwanza vilikuwa vimetoweka, nayo bahari pia haikuweko tena.
2 Nikaona mji mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka kwa Mungu
mbinguni. Ulikuwa umetayarishwa vizuri kama bibi arusi aliyepambwa
tayari kukutana na mumewe.
3 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka katika kiti cha enzi ikisema,
“Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu. Atakaa kati yao, nao
watakuwa watu wake, naye atakuwa Mungu wao.
4 Yeye atayafuta machozi yao yote; maana hakutakuwako tena na kifo,
wala uchungu, wala kilio, wala maumivu; maana ile hali ya kale
imepita!”

5 Kisha yule aliyeketi juu ya kiti cha enzi akasema, “Tazama,
nafanya yote mapya.” Tena akaniambia, “Andika hili, maana maneno haya
ni ya kuaminika na ya kweli!”
6 Kisha akaniambia, “Yametimia! Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na
Mwisho. Aliye na kiu nitampa kinywaji cha bure kutoka katika chemchemi
ya maji ya uzima.
7 Yeyote atakayeshinda atapokea hiki, nami nitakuwa Mungu wake, naye
atakuwa mwanangu.
8 Lakini watu waoga, wasioamini, wapotovu, wauaji, wazinzi, wachawi,
waabudu sanamu, na waongo wote, mahali pao patakuwa ndani ya lile ziwa
linalowaka moto na kiberiti; hicho ndicho kifo cha pili.”
\fr 21:7
\f taz Zab 89:26-27

Yerusalemu mpya

9 Kisha mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba
yaliyokuwa yamejaa mabaa saba ya mwisho, akaja na kuniambia, “Njoo!
Mimi nitakuonyesha bibi arusi, mkewe Mwanakondoo!”
10 Basi, Roho akanikumba, naye malaika akanipeleka juu ya mlima
mrefu sana. Akanionyesha mji mtakatifu, ukishuka kutoka kwa Mungu
mbinguni,
11 uking’aa kwa utukufu wa Mungu. Mwangaza wake ulikuwa kama wa jiwe
la thamani kubwa kama yaspi, angavu kama kioo.
12 Ulikuwa na ukuta mrefu na mkubwa, wenye milango kumi na miwili,
na malaika wanangojea kumi na wawili. Majina ya wangoja milango kumi na
mawili ya Israeli yalikuwa yameandikwa juu ya milango hiyo.
13 Kila upande ulikuwa na milango mitatu: upande wa mashariki,
milango mitatu, kaskazini milango mitatu, kusini milango mitatu na
magharibi milango mitatu.
14 Kuta za mji huo zilikuwa zimejengwa juu ya mawe ya msingi kumi na
mawili, na juu ya mawe hayo yalikuwa yameandikwa majina na mitume kumi
na wawili wa Mwanakondoo.

15 Basi, yule malaika aliyekuwa anasema nami alikuwa na kijiti cha
dhahabu cha kupimia, kwa ajili ya kuupima huo mji, milango yake na kuta
zake.
16 Mji wenyewe ulikuwa wa mraba, upana na urefu wake sawa. Basi,
malaika akaupima mji huo kwa kijiti chake: ulikuwa na urefu, upana na
urefu wa kwenda juu, kama kilomita elfu mbili na mia nne.
17 Kisha akaupima ukuta wake pia; nao ulikuwa mita sitini kwa kipimo
cha macho cha kibinadamu ambacho malaika alitumia.
18 Ukuta huo ulikuwa umejengwa kwa mawe mekundu ya thamani, na mji
wenyewe ulikuwa umejengwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.
19 Mawe ya msingi wa ukuta huo yalikuwa yamepambwa kwa kila aina ya
mawe ya thamani. Jiwe la kwanza la msingi lilikuwa jiwe la thamani
jekundu, la pili yakuti samawati, la tatu kalkedoni, la nne zamaradi,
20 la tano sardoniki, la sita akiki, la saba krisolito, la nane
zabarijadi, la tisa topazi, la kumi krisopraso, la kumi na moja yasinto,
na la kumi na mbili amethisto.
21 Na ile milango kumi na miwili ilikuwa lulu kumi na mbili; kila
mlango ulikuwa umetengenezwa kwa lulu moja. Barabara kuu ya mji ilikuwa
imetengenezwa kwa dhahabu safi, angavu kama kioo.

22 Sikuona hekalu katika mji huo, maana Bwana Mungu Mwenye Uwezo na
yule Mwanakondoo ndio Hekalu lake.
23 Mji huo hauhitaji jua wala mwezi kuangazia, maana utukufu wa
Mungu huuangazia, na taa yake ni yule Mwanakondoo.
24 Watu wa mataifa watatembea katika mwanga wake, na wafalme wa
dunia watauletea utajiri wao.
25 Milango ya mji huo itakuwa wazi mchana wote; maana hakutakuwa na
usiku humo.
26 Fahari na utajiri wa watu wa mataifa utaletwa humo ndani.
27 Lakini hakuna chochote kilicho najisi kitakachoingia humo; wala
mtu yeyote atendaye mambo ya kuchukiza au ya uongo hataingia humo. Ni
wale tu walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwanakondoo ndio
watakaoingia ndani.

\c 22

1 Kisha malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima maangavu kama kioo
yakitoka kwenye kiti cha enzi cha Mungu na Mwanakondoo.
2 Mto huo ulitiririka kupitia katikati ya barabara kuu ya mji.
Kandokando ya mto huo kulikuwa na mti wa uzima unaozaa matunda mara kumi
na mbili kwa mwaka, yaani kila mwezi; na majani yake ni dawa ya
kuwaponya watu wa mataifa.
3 Hapana kitu chochote kilicholaaniwa kitakachokuwa katika mji huo.
Kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwanakondoo kitakuwa katika mji huo,
na watumishi wake watamwabudu.
4 Watauona uso wake, na jina lake litaandikwa juu ya paji za nyuso
zao.
5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua,
maana Bwana Mungu atawaangazia, nao watatawala milele na milele.

Kuja kwa Yesu

6 Kisha malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kweli na ya
kuaminika. Bwana Mungu ambaye huwapa manabii Roho wake, alimtuma malaika
wake awaonyeshe watumishi wake mambo ambayo lazima yatukie punde.

7 “Sikiliza! Naja upesi. Heri yake anayeyazingatia maneno ya unabii
yaliyo katika kitabu hiki.”

8 Mimi Yohane, niliyaona na kusikia mambo haya. Nilipokwisha sikia
na kuona nikajitupa chini mbele ya miguu ya huyo malaika aliyenionyesha
mambo hayo, nikataka kumwabudu.
9 Lakini yeye akaniambia, “Acha! Mimi ni mtumishi tu kama wewe na
ndugu zako manabii na wote wanaoyatii maagizo yaliyomo katika kitabu
hiki. Mwabudu Mungu!”
10 Tena akaniambia, “Usiyafiche kama siri maneno ya unabii yaliyomo
katika kitabu hiki, maana wakati wa kutimizwa kwake umekaribia.
11 Kwa sasa anayetenda mabaya na aendelee kutenda mabaya, na aliye
mchafu aendelee kuwa mchafu. Mwenye kutenda mema na azidi kutenda mema,
na aliye mtakatifu na azidi kuwa mtakatifu.”
\fr 22:12
\f taz Zab 28:4

12 “Sikiliza!” Asema Yesu, “Naja upesi, pamoja na tuzo
nitakalompa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
13 Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho, wa kwanza na wa
mwisho.”

14 Heri yao wale wanaoosha mavazi yao, kwani watakuwa na haki ya
kula tunda la mti wa uzima, na haki ya kuingia mjini kwa kupitia milango
yake.
15 Lakini mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabudu sanamu na wote
wanaopenda kusema uongo, watakaa nje ya mji.

16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu awathibitishieni mambo haya
katika makanisa. Mimi ni mzawa wa ukoo wa Daudi. Mimi ni nyota angavu ya
asubuhi!”

17 Roho na Bibiarusi waseme, “Njoo!” Kila mtu asikiaye hili, na
aseme,”Njoo!” Kisha, yeyote aliye na kiu na aje; anayetaka maji ya
uzima na apokee bila malipo yoyote.

Hatima

18 Mimi Yohane nawapa onyo wote wanaosikia maneno ya unabii yaliyomo
katika kitabu hiki: mtu yeyote akiongeza chochote katika mambo haya,
Mungu atamwongezea mabaa yaliyoandikwa katika kitabu hiki.
19 Na mtu yeyote akipunguza chochote katika maneno ya unabii
yaliyomo katika kitabu hiki, Mungu atamnyang’anya sehemu yake katika ule
mti wa uzima, na sehemu yake katika mji mtakatifu, ambavyo vimeelezwa
katika kitabu hiki.
20 Naye anayetoa ushahidi wake juu ya mambo haya asema: “Naam! Naja
upesi.”
Amina. Na iwe hivyo! Njoo Bwana Yesu!

21 Nawatakieni nyote neema ya Bwana Yesu. Amen.